Jumapili, 25 Machi 2018

111: Kama hakusaidii achana naye!



Mpendwa Msomaji wa makala za “ujasiriamaliafya”, Salaam!
Baada ya salaam napenda leo tuangalie eneo moja la ni yupi rafiki wa muhimu na yupi si rafiki wa muhimu. Kwanza kabisa ni muhimu kufahamu kila binadamu anayo thamani kubwa sana kwa kuwepo kwake hapa duniani ingawa si kila binadamu anaweza kuwa rafiki yako. Neno rafiki au kiingereza “friend” ni mtu ambaye kwa namna yeyote atakuwa ni mtu wako wa karibu katika furaha na huzuni. Atakuwa ni mtu anayependa kukuona unafanikiwa na kuendelea mbele. Na hapa haijalishi kwamba unalingana naye umri au ni mdogo kuliko wewe au mkubwa kuliko wewe.
Rafiki anaweza kutoka katika kundi lolote iwe kazini, katika eneo lako la biashara au mahali popote, muhimu kuangalia jee anakidhi vigezo vya kuwa mtu wangu wa karibu katika dhiki au katika furaha au mawazo yake yananifanya nisonge mbele!???. Fahamu jambo moja hapa rafiki kwa vigezo tunavyoangalia leo ni zaidi ya ndugu, mke au mume wako.
Watu wengi utaona wanatunza namba nyingi sana katika simu zao na utaona hata kuzipoteza hawako tayari, kwamba wacha niwe nazo tuu. Swali la kujiuliza jee namba za simu zote ulizozitunza ni za marafiki zako au watu baki tuu!? Kuwa na kundi kubwa ambalo kimsingi siyo marafiki zako ni kujichelewesha kimaendeleo na kupoteza muda wako ambao kama ungeutumia vizuri matokeo yangekuwa yakushangaza.
Ili uweze kwenda kwa kukimbia na siyo kutembea, leo ninakushauri achana na marafiki wasikuwa wa msaada kwako kwani hao ni mizigo inayokufanya usikimbie katika mafanikio yako na zaidi waweza kurudishwa nyuma.
Leo tuchukue muda wa kutafakari umuhimu wa kila unayemuita rafiki yako na kama hakusaidii mfute na mpotezee kwani hakusaidii!!! Ili kufikia mafanikio makubwa na malengo ambayo umekuwa ukiota ndoto ya kuyafikia wakati wote, muhimu ni kupunguza marafiki wasio na msaada kwako. Na baada ya kuwapunguza imarisha na ongeza nguvu kubwa zaidi ya kuwashikilia hao wachache ambao umetambua ya kuwa ndio marafiki zako.
Nakutakia siku njema!
Mtega GFA
CEO – UjasiriamaliAfya

Hakuna maoni: