Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo Afya. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo Afya. Onyesha machapisho yote

Jumapili, 27 Agosti 2017

AFYA YA UZAZI KWA VIJANA



     SOMO: KWA NINI ELIMU YA KINA YA UJINSIA, MAADILI YA AFYA NA STADI ZA MAISHA [Comprehensive Sexuality Education – CSE]?
Ø  Inawawezesha Vijana balehe kujizuia na mimba zisizotarajiwa na maambukizo kwa njia ya ngono, ikiwa ni pamoja na VVU.
Ø  Inawasaidia Vijana balehe kufanya maamuzi sahihi hasa ya kuchelewa kuanza kufanya ngono na ukatili wa kijinsia.
Ø  Ina hamasisha Vijana balehe kuwa na uhusiano unaofaa zaidi na wenye Afya pamoja na kupunguza ukatili wa kijinsia, uonevu na ubaguzi.
KWA NINI HUDUMA ZA UJINSIA NA AFYA YA UZAZI – Sexuality Reproductive Health?
Vijana balehe wanahitaji kupata elimu salama, za gharama nafuu na zinazokubalika kulingana na viwango vya Kimataifa vya Huduma Rafiki za Afya ya Uzazi kwa Vijana.
Serikali zinawajibu wa kutoa huduma hizi kwa sababu:
Ø  Kutimiza haki ya afya ya umma kulinda afya ya kizazi kijacho.
Ø  Zitolewe kwa pamoja na huduma nyingine za elimu ya ujinsia, afya ya uzazi, maadili ya afya na stadi za maisha zenye ufanisi zaidi.
Ø  Kuhakikisha kwamba Vijana balehe wanajisikia salama na kujiamini katika upatikanaji wa huduma.
Ø  Kupunguza mimba zisizotarajiwa, VVU, magonjwa mengine ya ngono na kuboresha kiwango cha kuishi kwa wajawazito na watoto hatimaye kuliletea Taifa letu maendeleo makubwa sana.


                                        VIJANA WA LEO.
HALI HALISI YA AFYA YA UZAZI KWA VIJANA TANZANIA
VIJANA NI IDADI KUBWA YA WANANCHI TANZANIA
UJANA ni umri kati ya miaka 10 hadi 24. Ni kipindi cha mpito kati ya utoto na utu uzima ambapo vijana wanapitia mabadiliko mengi ya ukuaji na kiafya.
RIPOTI YA TAFITI ZA DEMOGRAFIA NA AFYA ZA 2010.
·         Tanzania ilikuwa na jumla ya watu milioni 43.2 [ 43,187 823 ], Vijana milioni 14 = 31%

MATATIZO YA VIJANA YA AFYA YA UZAZI

1.    Wasichana wengi huanza kujihusisha na ngono kwa wastani wakiwa na umri wa miaka 17 wakati wavulana miaka 15
2.    Vijana wengi huanza kujihusisha na mapenzi kabla ya kuingia kwenye ndoa.
3.     32% ya wasichana wasioolewa na wavulana  42% wasiooa wa umri wa miaka  14 -20 walishaanza kujamiana.
4.    9% ya wasichana na 10% ya wavulana wa miaka 15 – 20 walishaanza kujamiana kabla ya kutimiza umri wa miaka 15.
5.    Inakadiriwa kuwa  65% ya wasichana wafikapo umri wa miaka 18 tayari huwa wameshaanza kujamiiana.
6.    18% ya wasichana wenye umri  wa  miaka 15 – 19 tayari                                                                wameshaolewa na 37% ya wasichana wenye umri wa miaka 20 – 24 waliolewa   au kuwa kwenye unyumba walipokuwa na umri wa      miaka 18.
7.    4% ya wavulana wenye umri kati ya miaka 15 -19 wameshaoa. Ndoa za utotoni hutokea kwa kiwango kikubwa katika Mikoa ya Shinyanga ambapo 59% ya wasichana wenye umri wa miaka 15 -19 walishaolewa na mkoa wa Mara ni 55%.Kuolewa katika umri chini ya miaka 20 ni kuwaweka wasichana katika hatari ya kupata mimba za utotoni.
                                     
Ø  Mimba katika umri mdogo ni tatizo kubwa mojawapo la Afya ya Uzazi hapa nchini.
Ø  23% ya wasichana wenye umri wa miaka 15 – 19 wamekwisha zaa watoto hai au wana mimba ya kwanza ambapo 6% wana ujauzito wa kwanza.
Ø  Wasichana 116 kati ya 1000 wenye umri kati ya miaka 10 – 19 wana watoto tayari.
Ø  Ni 16% tu ya wasichana wenye umri wa miaka 15 – 24 wanatumia njia za kisasa za uzazi wa mpango.
Ø  22% ya wasichana wanataka kutumia njia za uzazi wa mpango lakini wanashindwa kupata huduma hizo.

WASICHANA KUPATA MIMBA KATIKA UMRI MDOGO

v  Ni tatizo kubwa sana la afya ya uzazi nchini.
v  23% ya wasichana wenye umri wa kati ya 15 -19 wamekwisha zaa mtoto hai au wana mimba.
v  52% ya wasichana wenye umri wa miaka 15 -19 hawana elimu ya sekondari kutokana na kuapata mimba ama watoto.
v  Mimba za utotoni huchangia vifo vingi vya wajawazito na watoto.
v  Watoto waliozaliwa na wasichana wenye umri mdogo wananafasi    ndogo ya kuishi kufikia miaka 5 ikilinganishwa na wale wanao               zaliwa na wanawake wenye umri mkubwa.
v  Wasichana 111 kwa 1000 wenye umri chini ya miaka 20 hupoteza watoto wao tofauti na vifo vya watoto waliozaliwa na wanawake wenye umri  kati ya miaka 30 hadi 39 ambapo ni 93 kwa 1000.

UTOAJI MIMBA.
Vifo ni 16%, wengi wao ni vijana.

MATATIZO YA KUJAMIIANA KATIKA UMRI MDOGO.

Kwa Msichana
A.   Kukatiza masomo na kuathirika kimaisha.
B.   Kukataliwa na familia.
C.   Kupata matatizo wakati wa kujifungua.
D.   Kifo
Kwa Mvulana:
A.   Kukatiza masomo na kuathirika kimaisha.
B.   Kufunga ndoa za kulazimishwa.
C.   Kukosa uwezo wa kulea familia.
Kwa mtoto:
Ø  Kuzaliwa na uzito pungufu.
Ø  Kuzaliwa mtoto njiti.
Ø  Kupata matatizo wakati wa kuzaliwa
Ø  Kukosa mapenzi kwa wazazi.
Ø  Kifo

VIJANA NA MAAMBUKIZO YA VVU/UKIMWI
v  UKIMWI ni ugonjwa unaosababishwa na Virusi Vya UKIMWI [VVU/ HIV] vinavyodhoofisha kinga ya mwili ya kujikinga na maradhi mbalimbali.

JINSI UKIMWI UNAVYOENEZWA.
Ø  90% ya maambukizo ni kwa njia ya kujamiiana na mtu mwenye VVU.
Ø  Mama mwenye VVU anaweza kumwambukiza mototo wake wakati wa:
a.   Ujauzito.
b.   Uchungu na kujifungua.
c.    Kunyonyesha
d.   Kuchangia damu yenye VVU.

ü  Karibu 1/2 ya wasichana na 1/3 ya wavulana wamewahi kupimwa VVU na kupokea majibu yao.
ü   Vijana wa miaka 15 – 24 huchangia kwa 2% ya maambukizi mapya ya VVU Tanzania.
ü  Vijana walio kwenye ndoa au wanaishi na wenza maambukizi ya VVU ni 2.6% ikilinganishwa na 1.4% ya ambao hawako kwenye ndoa.
ü  Maambukizi mapya ya VVU ni 45% kwa wasichana wenye umri kati ya miaka 15 – 24 wakati wanaume ni 26% kwa umri huo.
ü  Magonjwa ya ngono yanaongeza kasi ya maambukizo ya VVU.

MAGONJWA YATOKANAYO NA KUJAMIANA.
Magonjwa yanayo ambukizwa kwa njia ya tendo la kujamiiana na mtu  ni miongoni mwa magonjwa haya;
Ø  Kisonono
Ø  Klamidia
Ø  Trichomoniasis
Ø  Kaswende
Ø  Herpes
Ø  Pangusa – Chancroid
Ø  Virusi Vya UKIMWI

NAMNA YA KUJIKINGA NA MIMBA.
v  Kuacha kabisa kujamiana.
v  Tumia kondomu kila wakati na kwa usahihi.
v  Tumia njia ya uzazi wa mpango uliyoichagua kuzuia mimba.

NAMNA YA KUEPUKA TENDO LA KUJAMIIANA AMBALO SI SALAMA NA SI LAZIMA KWA WASIO NA NDOA.
ü  Epuka kujamiiana katika umri mdogo, kama ulishaanza acha mara moja.
ü  Epuka ulevi wa aina yoyote ile
ü  Shiriki katika michezo mbalimbali ili kupambana na mihemko ya mwili wako.
ü  Endapo utashindwa kujizuia kabisa unashauriwa kutumia kondomu kwa usahihi.
ü  Kondomu ikitumika kwa usahihi kwa kila tendo la kujamiiana huzuia mimba, maambukizo ya VVU na  magonjwa ya ngono.
ü  Epuka kushirikiana na rafiki mpenda ngono,kuomba omba/  kupewa zawadi mbalimbali na vishawishi vingine vingi ambavyo vitasababisha uingie katika ngono.
ü  Usifanye rushwa ya ngono, ni kosa la kisheria.
ü  Epuka tabia ya uvivu.
ü  Usishiriki michezo na mikesha ya usiku isiyo ya lazima.
ü  Enzi Mafundisho ya dini yako kwani ni mafundisho yanayo kataza zinaa.

TAHADHARI kwa Wasichana:
     Wanaweza kupata mimba
v  Kabla ya kupata hedhi.
v  Bila kufanya tendo la kujamiiana endapo katika hali ya mapenzi mvulana atamwaga shahawa karibu na UKE.
v  Wanapofanya tendo la kujamiiana kwa mara ya kwanza.
           
NJIA ZA UZAZI WA MPANGO:
a] Za muda mfupi:
      > Vidonge vyenye Vichocheo Viwili
      >      ,,              ,, kichocheo kimoja [POPS]
     > Dawa Za Povu Na Jeli [Spermicides]
      > Njia ya Ute [BOM]
      > Kunyonyesha Tu [LAM]

b] Za muda mrefu:
     > Sindano [ Depo Provena ]
     > Vipandikizi [ Norplant ]
     > Kitanzi [ IUCD ]
AFYA YA UZAZI NA MALEZI KWA VIJANA BALEHE.

C] Njia za kudumu:
      > Kufunga uzazi mwanaume [ Vasectomy ]
      > Kufunga uzazi mwanamke  [ BTL ]

Marejeo:           
1.    Youth in Tanzania – data from the 2010 Tanzania Demographic and Health Survey ( TDHS ).
2.    Vijana Wa Leo handouts – Wizara ya afya na U/Jamii.
3.    National Adolescent Reproductive Health Strategy 2011 – 2015.
4.    Wizara ya Afya na U/Jamii, Kitengo Cha Afya ya Uzazi na Mtoto, barua pepe:Afya_promo@moh.go.tz
      

Jumatano, 2 Agosti 2017

MWONGOZO WA ULAJI BORA KWA WATU WANAOISHI NA VIRUSI VYA UKIMWI NA WENYE UKIMWI.



SEHEMU YA KWANZA:    MLO KAMILI.
Utangulizi.
Ujasiriamali unategemea sana uimara wa afya yako. Ni kwa msingi huo leo tutaangalia muongozo wa ulaji kwa watu waishio na UKIMWI/WAVIU.
Lishe ni mahitaji ya msingi kwa binadamu wote. Magonjwa sugu huzuia mmeng’enyo wa wa chakula mwilini, husababisha mtu kukosa hamu ya kula na hivyo kusababisha utapiamlo. Kwa WAVIU na magonjwa mengine sugu,mahitaji ya lishe kwenye mwili ni makubwa wakati dalili za mwanzo hazijaanza kuonekana. Hatari yakupata utapiamlo inaongezeka katika kipindi cha ugonjwa. Lishe bora siyo tiba bali ni kinga dhidi ya maambukizo. Lishe bora huongeza kinga pamoja na ubora wa maisha.

Nini maana ya mlo kamili?
Jibu:   Mlo kamili ni ule wenye mchanganyiko wa vyakula kutoka makundi mbalimbali. Mlo huo huwa na virutubishi vyote muhimu na kwa kiasi kinachotosheleza kwa afya bora ya mlaji.Ni muhimu sana vyakula hivi viliwe kwa wakati mmoja ili kuuwezesha mwili kutumia virutubishi mbalimbali kwa ufanisi. Kwa mfano, Vitamini C husaidia ufyonzwaji wa madini ya chuma yanayo patikana kwenye vyakula vyenye asili ya mimea, pia mafuta husaidia ufyonzwaji wa  vitamin A, D,E na K. Hakikisha kwamba milo miwili(2) hadi mitatu(3) kwa siku iwe milo kamili.

Maana ya Lishe:
Lishe ni sayansi ya matumizi ya virutibisho kwenye mwili wa binadamu kwa ajili ya maendeleo, ukuaji, uzalishaji na utunzaji wa afya.

Kwa nini  ule mlo kamili?
Ø  Huwezesha mwili kupata virutubishi vyote vinavyohitajika kwa wakati mmoja.
Ø  Huboresha kinga ya mwili dhidi ya maradhi mbalimbali.
Ø  Humpa mtu nguvu za kufanya kazi mbalimbali.
Ø  Huuwezesha mwili kutumia virutubishi mbalimbali kwa ufanisi. Kwa mfano, Vitamini C husaidia ufyonzwaji wa madini ya chuma yanayo patikana kwenye vyakula vyenye asili ya mimea, pia mafuta husaidia ufyonzwaji wa vitamin A, D,E na K.
KUMBUKA:
Tumia vyakula vinavyopatikana kwenye mazingira unayoishi.
Ø  Tumia vyakula vya asili ikiwa ni pamoja na mboga-mboga, matunda pori na wadudu wanaoliwa.
Ø  Kula matunda na mboga-mboga katika kila mlo.
Ø  Badili aina ya vyakula kila inapowezekana.
Ø  Chakula cha kutosha huuwezesha mwili kukidhi ongezeko la mahitaji ya virutubishi.
Ø  Kula milo miwili(2) hadi mitatu(3) iliyo kamili na asusa (vitafunwa) kati ya mlo na mlo.
Ø  Kula milo midogo midogo mara nyingi, endapo huwezi kula chakula cha kutosha kwa mara moja.
Ø  Zingatia usafi na usalama wa chakula na maji.
Ø  Tumia mafuta na sukari kwa kiasi.
Ø  Punguza matumizi ya chumvi.
Ø   Kahawa, kokoa, chai, chokoleti na baadhi ya soda vina kafeini ambayo huzuia ufonzwaji wa madini ya chuma yanayopatikana kwenye vyakula vya mimea.

Ø   Mtu mwenye VVU/ UKIMWI inapobidi anaweza kutumia kwa kiasi kidogo angalau saa moja kabla au baada ya kula.
Ø  Epuka kutumia pombe na sigara kwa sababu vinaingilia matumizi ya chakula na virutubishi, na pia huchangia kupunguza kinga ya mwili. Kadhalika hukuongezea hatari ya kupata magonjwa sugu kama saratani ya kinywa, koromeo na ini na hata kifua kikuu.
Ø  Fanya mazoezi ya mwili kama shuguli za nyumbani, kazi za bustani au kutembea ili kuboresha matumizi ya chakula mwili na kujenga misuli.
Ø  Aina ya mazoezi hutegemea hali ya mgonjwa.
SEHEMU YA PILI.
Mlo kamili unatakiwa kuwa na chakula angalau kimoja kutoka katika makundi yafuatayo ya vyakula na vyakula hivyo viliwe pamoja.

1 .KUNDI LA KWANZA
Nafaka, mizizi na ndizi za kupika.
·         Mazao ya nafaka ni; mahindi, ulezi, ngano, mtama,mpunga, uwele na shayiri.
·         Mazao ya mizizi ni; viazi vitamu, viazi mviringo, viazi vikuu, magimbi, mhogo na vyakula vingine vingi vya mizizi.
·         Ndizi mbichi za kupika ambazo hazijaanza kuiva.
Vyakula vya kundi hili huchukua sehemu kubwa ya mlo ambapo kazi yake kubwa ni kuupa mwili nguvu na joto, pia huupa mwili kiasi        kidogo cha madini, vitamini na utomwili ( protini ).
2. KUNDI LA PILI.
Vyakula vya jamii ya mikunde, vile vyenye kokwa na vyenye  asili ya wanyama:
Jamii ya mikunde ni;
·         Maharage, njegere, kunde; soya, njugumawe, dengu, mbaazi, fiwi na choroko.
Vyenye kokwa ni;
·         Karanga, korosho, kweme na kokwa za asili zinazo toa mafuta.

Vyemye asili ya wanyama ni;
·         Nyama, samaki, dagaa, senene, maziwa, jibini, mayai, nzige na kumbikumbi na wadudu wengine wanaoliwa. Vyakula vya kundi hili huupatia mwili utomwili (protini ) na kiasi kidogo cha vitamini na madini.
·         Kazi ya protini ni kukarabati na kukuza mwili.

3. KUNDI LA TATU.
Mboga-mboga:
·         kundi hili linajumuisha aina zote za mboga za majani (mboga za kupandwa na mboga pori) kama mchicha, matembele, majani ya kunde, majani ya maharage, mnafu, mchunga, bamia, pilipili hoho, karoti, bilinganya, maboga, matango, bitiruti na mboga mbalimbali za asili.
  • Mboga-mboga huupatia mwili vitamini na madini kwa wingi ambavyo kazi yake kubwa sana ni kuboresha kinga ya mwili hasa kwa watu wanaoishi na VVU /UKIMWI
4.KUNDI LA NNE.
Matunda:
  • Kundi hili linajumuisha aina zote za matunda kama pera, papai, embe, chungwa, karakara (pesheni ), limau, ndimu, chenza, parachichi, ndizi mbivu, nanasi, pichesi, stafeli, fenesi, zambarau, topetope na matunda pori yaliwayo kama vile ukwaju, ubuyu, mabungo, embe ng’ong’o,  nk.
5. KUNDI LA TANO.
Mafuta na Sukari.    
Mafuta na sukari huongeza nishati-lishe (nguvu) na uzito wa mwili, pia huupa mwili joto. Vyakula hivi pia huongeza ladha ya vyakula. Pia mafuta hulainisha vyakula na kusaidia uyeyushwaji na usharabu wa baadhi ya virutubishi kama A, D, E na K. Vyanzo vya mafuta ni:
Mafuta yatokanayo na mimea ni:
·      Korosho, ufuta, alizeti, kweme, karanga, nazi, mbegu za maboga, mafuta ya mawese na mbegu za mimea ya porini.
Mafuta yatokanayo na wanyama:
·                              Samli, siagi, mafuta ya nyama yenyewe na mafuta ya samaki.

Sukari:
·         Sukari yenyewe, sukari gulu, miwa na asali.

Maji.

Japo siyo kundi la chakula lakini ni sehemu muhimu ya mlo. Maji ni muhimu kwa kurekebisha joto la mwili na kusaidia mfumo wa chakula. Ili mwili ufanye kazi yake vizuri kwa uhai unahitaji uwepo wa maji. Nimuhimu kunywa maji angalau lita 1.5(glasi 8) kwa siku. Ni muhimu sana kunywa maji safi na salama.


MFANO WA RATIBA YA MLO KAMILI KWA WAVIU.

MUDA WA KULA CHAKULA
AINA YA CHAKULA

1

Saa  1: 30 Asubuhi.
Uji wa mahindi uliochanganywa  karanga na dagaa.






2

Saa  4: 30 Asubuhi.
Chai, yai la kuchemshwa, parachichi na viazi vilivyoungwa karanga.







3

Saa 7: 30 Mchana.
Ugali wa mahindi, Njegele, Mboga ya matembele imeungwa kwa mafuta ya alizeti, Parachichi.





4
Saa 10: 30 Mchana.
Karanga zilizo kaangwa za kutafuna na maji ya matunda.






5

Saa 1: 30 Usiku


Ndizi zilizo pikwa pamoja  na bamia na nyama, Mchicha, Chungwa.





6
Saa 4: 00 Usiku
Kachumbali.

Hakikisha kwamba milo miwili(2) hadi mitatu(3) kwa siku iwe milo kamili.
Pamoja na ulaji bora uliotajwa hapo juu mgonjwa au mtu anayeishi na VVU anapaswa kufanya yafuatayo:
a.       Aepuke kupata maambukizo mapya.
b.      Aepuke kuwaambukiza watu wengine.
c.       Afanye kazi za kipimo/asifanye kazi ngumu.
d.      Apate mapumuziko ya kutosha.
e.       Afanye mazoezi ya viungo kwa kutembea n.k.
f.       Asitumie pombe aina yoyote wala kuvuta sigara.
g.      Azingatie usafi wa mwili, mavazi, mahali pa kulala na mazingira yake.
h.      Anywe maji safi na salama.
i.        Ashiriki shughuli mbalimbali za kijamii, kiuchumi na maendeleo.



Imendaliwa na;

Leslie Mhagama
0763 90 10 46
lesliemhagama@gmail.com