Jumatano, 2 Agosti 2017

MWONGOZO WA ULAJI BORA KWA WATU WANAOISHI NA VIRUSI VYA UKIMWI NA WENYE UKIMWI.



SEHEMU YA KWANZA:    MLO KAMILI.
Utangulizi.
Ujasiriamali unategemea sana uimara wa afya yako. Ni kwa msingi huo leo tutaangalia muongozo wa ulaji kwa watu waishio na UKIMWI/WAVIU.
Lishe ni mahitaji ya msingi kwa binadamu wote. Magonjwa sugu huzuia mmeng’enyo wa wa chakula mwilini, husababisha mtu kukosa hamu ya kula na hivyo kusababisha utapiamlo. Kwa WAVIU na magonjwa mengine sugu,mahitaji ya lishe kwenye mwili ni makubwa wakati dalili za mwanzo hazijaanza kuonekana. Hatari yakupata utapiamlo inaongezeka katika kipindi cha ugonjwa. Lishe bora siyo tiba bali ni kinga dhidi ya maambukizo. Lishe bora huongeza kinga pamoja na ubora wa maisha.

Nini maana ya mlo kamili?
Jibu:   Mlo kamili ni ule wenye mchanganyiko wa vyakula kutoka makundi mbalimbali. Mlo huo huwa na virutubishi vyote muhimu na kwa kiasi kinachotosheleza kwa afya bora ya mlaji.Ni muhimu sana vyakula hivi viliwe kwa wakati mmoja ili kuuwezesha mwili kutumia virutubishi mbalimbali kwa ufanisi. Kwa mfano, Vitamini C husaidia ufyonzwaji wa madini ya chuma yanayo patikana kwenye vyakula vyenye asili ya mimea, pia mafuta husaidia ufyonzwaji wa  vitamin A, D,E na K. Hakikisha kwamba milo miwili(2) hadi mitatu(3) kwa siku iwe milo kamili.

Maana ya Lishe:
Lishe ni sayansi ya matumizi ya virutibisho kwenye mwili wa binadamu kwa ajili ya maendeleo, ukuaji, uzalishaji na utunzaji wa afya.

Kwa nini  ule mlo kamili?
Ø  Huwezesha mwili kupata virutubishi vyote vinavyohitajika kwa wakati mmoja.
Ø  Huboresha kinga ya mwili dhidi ya maradhi mbalimbali.
Ø  Humpa mtu nguvu za kufanya kazi mbalimbali.
Ø  Huuwezesha mwili kutumia virutubishi mbalimbali kwa ufanisi. Kwa mfano, Vitamini C husaidia ufyonzwaji wa madini ya chuma yanayo patikana kwenye vyakula vyenye asili ya mimea, pia mafuta husaidia ufyonzwaji wa vitamin A, D,E na K.
KUMBUKA:
Tumia vyakula vinavyopatikana kwenye mazingira unayoishi.
Ø  Tumia vyakula vya asili ikiwa ni pamoja na mboga-mboga, matunda pori na wadudu wanaoliwa.
Ø  Kula matunda na mboga-mboga katika kila mlo.
Ø  Badili aina ya vyakula kila inapowezekana.
Ø  Chakula cha kutosha huuwezesha mwili kukidhi ongezeko la mahitaji ya virutubishi.
Ø  Kula milo miwili(2) hadi mitatu(3) iliyo kamili na asusa (vitafunwa) kati ya mlo na mlo.
Ø  Kula milo midogo midogo mara nyingi, endapo huwezi kula chakula cha kutosha kwa mara moja.
Ø  Zingatia usafi na usalama wa chakula na maji.
Ø  Tumia mafuta na sukari kwa kiasi.
Ø  Punguza matumizi ya chumvi.
Ø   Kahawa, kokoa, chai, chokoleti na baadhi ya soda vina kafeini ambayo huzuia ufonzwaji wa madini ya chuma yanayopatikana kwenye vyakula vya mimea.

Ø   Mtu mwenye VVU/ UKIMWI inapobidi anaweza kutumia kwa kiasi kidogo angalau saa moja kabla au baada ya kula.
Ø  Epuka kutumia pombe na sigara kwa sababu vinaingilia matumizi ya chakula na virutubishi, na pia huchangia kupunguza kinga ya mwili. Kadhalika hukuongezea hatari ya kupata magonjwa sugu kama saratani ya kinywa, koromeo na ini na hata kifua kikuu.
Ø  Fanya mazoezi ya mwili kama shuguli za nyumbani, kazi za bustani au kutembea ili kuboresha matumizi ya chakula mwili na kujenga misuli.
Ø  Aina ya mazoezi hutegemea hali ya mgonjwa.
SEHEMU YA PILI.
Mlo kamili unatakiwa kuwa na chakula angalau kimoja kutoka katika makundi yafuatayo ya vyakula na vyakula hivyo viliwe pamoja.

1 .KUNDI LA KWANZA
Nafaka, mizizi na ndizi za kupika.
·         Mazao ya nafaka ni; mahindi, ulezi, ngano, mtama,mpunga, uwele na shayiri.
·         Mazao ya mizizi ni; viazi vitamu, viazi mviringo, viazi vikuu, magimbi, mhogo na vyakula vingine vingi vya mizizi.
·         Ndizi mbichi za kupika ambazo hazijaanza kuiva.
Vyakula vya kundi hili huchukua sehemu kubwa ya mlo ambapo kazi yake kubwa ni kuupa mwili nguvu na joto, pia huupa mwili kiasi        kidogo cha madini, vitamini na utomwili ( protini ).
2. KUNDI LA PILI.
Vyakula vya jamii ya mikunde, vile vyenye kokwa na vyenye  asili ya wanyama:
Jamii ya mikunde ni;
·         Maharage, njegere, kunde; soya, njugumawe, dengu, mbaazi, fiwi na choroko.
Vyenye kokwa ni;
·         Karanga, korosho, kweme na kokwa za asili zinazo toa mafuta.

Vyemye asili ya wanyama ni;
·         Nyama, samaki, dagaa, senene, maziwa, jibini, mayai, nzige na kumbikumbi na wadudu wengine wanaoliwa. Vyakula vya kundi hili huupatia mwili utomwili (protini ) na kiasi kidogo cha vitamini na madini.
·         Kazi ya protini ni kukarabati na kukuza mwili.

3. KUNDI LA TATU.
Mboga-mboga:
·         kundi hili linajumuisha aina zote za mboga za majani (mboga za kupandwa na mboga pori) kama mchicha, matembele, majani ya kunde, majani ya maharage, mnafu, mchunga, bamia, pilipili hoho, karoti, bilinganya, maboga, matango, bitiruti na mboga mbalimbali za asili.
  • Mboga-mboga huupatia mwili vitamini na madini kwa wingi ambavyo kazi yake kubwa sana ni kuboresha kinga ya mwili hasa kwa watu wanaoishi na VVU /UKIMWI
4.KUNDI LA NNE.
Matunda:
  • Kundi hili linajumuisha aina zote za matunda kama pera, papai, embe, chungwa, karakara (pesheni ), limau, ndimu, chenza, parachichi, ndizi mbivu, nanasi, pichesi, stafeli, fenesi, zambarau, topetope na matunda pori yaliwayo kama vile ukwaju, ubuyu, mabungo, embe ng’ong’o,  nk.
5. KUNDI LA TANO.
Mafuta na Sukari.    
Mafuta na sukari huongeza nishati-lishe (nguvu) na uzito wa mwili, pia huupa mwili joto. Vyakula hivi pia huongeza ladha ya vyakula. Pia mafuta hulainisha vyakula na kusaidia uyeyushwaji na usharabu wa baadhi ya virutubishi kama A, D, E na K. Vyanzo vya mafuta ni:
Mafuta yatokanayo na mimea ni:
·      Korosho, ufuta, alizeti, kweme, karanga, nazi, mbegu za maboga, mafuta ya mawese na mbegu za mimea ya porini.
Mafuta yatokanayo na wanyama:
·                              Samli, siagi, mafuta ya nyama yenyewe na mafuta ya samaki.

Sukari:
·         Sukari yenyewe, sukari gulu, miwa na asali.

Maji.

Japo siyo kundi la chakula lakini ni sehemu muhimu ya mlo. Maji ni muhimu kwa kurekebisha joto la mwili na kusaidia mfumo wa chakula. Ili mwili ufanye kazi yake vizuri kwa uhai unahitaji uwepo wa maji. Nimuhimu kunywa maji angalau lita 1.5(glasi 8) kwa siku. Ni muhimu sana kunywa maji safi na salama.


MFANO WA RATIBA YA MLO KAMILI KWA WAVIU.

MUDA WA KULA CHAKULA
AINA YA CHAKULA

1

Saa  1: 30 Asubuhi.
Uji wa mahindi uliochanganywa  karanga na dagaa.






2

Saa  4: 30 Asubuhi.
Chai, yai la kuchemshwa, parachichi na viazi vilivyoungwa karanga.







3

Saa 7: 30 Mchana.
Ugali wa mahindi, Njegele, Mboga ya matembele imeungwa kwa mafuta ya alizeti, Parachichi.





4
Saa 10: 30 Mchana.
Karanga zilizo kaangwa za kutafuna na maji ya matunda.






5

Saa 1: 30 Usiku


Ndizi zilizo pikwa pamoja  na bamia na nyama, Mchicha, Chungwa.





6
Saa 4: 00 Usiku
Kachumbali.

Hakikisha kwamba milo miwili(2) hadi mitatu(3) kwa siku iwe milo kamili.
Pamoja na ulaji bora uliotajwa hapo juu mgonjwa au mtu anayeishi na VVU anapaswa kufanya yafuatayo:
a.       Aepuke kupata maambukizo mapya.
b.      Aepuke kuwaambukiza watu wengine.
c.       Afanye kazi za kipimo/asifanye kazi ngumu.
d.      Apate mapumuziko ya kutosha.
e.       Afanye mazoezi ya viungo kwa kutembea n.k.
f.       Asitumie pombe aina yoyote wala kuvuta sigara.
g.      Azingatie usafi wa mwili, mavazi, mahali pa kulala na mazingira yake.
h.      Anywe maji safi na salama.
i.        Ashiriki shughuli mbalimbali za kijamii, kiuchumi na maendeleo.



Imendaliwa na;

Leslie Mhagama
0763 90 10 46
lesliemhagama@gmail.com

Hakuna maoni: