Jumamosi, 15 Julai 2017

SHERIA YA URITHI

"Mwisho wa uongozi au utawala wako, waliobaki watakukumbuka kwa maendeleo uliyosababisha na kuwaachia" Je unataka watu wazungumze nini katika msiba wako?
Swali hili linaweza kuonekana si swali la kufurahisha miongoni mwa wasomaji wa makala za ujasiriamali afya, lakini ndugu yangu hebu siku ya leo tuchukue dakika chache tukiwa kama viongozi na watawala kujiuliza na kujitathimini kila mmoja kwa nafasi yake.
Katika maisha ya kawaida utaona mtu ambaye ni mzee au umri wake umeendelea sana anafanya vitu vya maendeleo ambavyo muda wa kupata matokeo yake itachukua miaka mingi sana, na atabezwa kwamba anatafuta nini wakati umri umekwisha!? Jibu rahisi ni kwamba anajijengea sifa na tabia ambayo itadumu baada ya yeye kutoweka duniani.
Kujenga sifa na tabia ambayo baada yako itakumbukwa imekuwa ni dhahiri hasa kwa Nchi yetu ya Tanzania ambapo tumeshuhudia mara nyingi Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Raisi John Magufuli akisema, "ninatengeneza mazingira ambayo watawala watakaokuja baada yangu wajionee fahari kuwa wakuu katika Taifa la Tanzania" hapa akimaanisha mabadiliko na tabia anayoijenga ndani ya utawala wake ni kwa vizazi vijavyo.
Tabia hii inapaswa kujengeka ndani ya kila mmoja anayejiita ni kiongozi au mtawala, kwamba ni katika familia, taasisi ya kidini au jamii. Kumbuka ipo siku utatoweka duniani au utatoka katika nafasi uliyo nayo sasa! na baada yako au yangu yupo atakaye fuatia au atakaye keti katika kiti chako. Na baada yako au yangu itabakia mifano ya vitu tulivyovifanya katika utawala au uhai wetu aidha watakuwepo watu tuliowawezesha ambao watatenda yale tuliyowarithisha.
Maxwell anasema, " mafanikio yakuja pale tunapofanya mambo makubwa miongoni mwetu, na maendeleo yanakuja pale wale tunaowawezesha wanapofanya kwa mfano wetu mambo makubwa kwa niaba yetu, umuhimu huja pale tunapozalisha viongozi ambao watafanya vitu vikubwa pamoja nasi, na urithi ni pale viongozi au watawala wanapowekwa katika nafasi kufanya mambo makubwa pasipo sisi kuwepo".
Na akamalizia kwa kusema, "uwezo wetu kama viongozi na watawala hautapimwa kwa majengo makubwa tuliyoyajenga, au taasisi tulizozianzisha, au vitu tulivyovifanya kwa umoja wetu katika kipindi cha uongozi au utawala au uhai wetu. Mimi na wewe tutapimwa kwa uwekezaji tulioufanya ndani ya watu ambao tutawaachia nafasi hii tuliyonayo kwasasa".
Mpendwa msomaji, hii ni changamoto ambayo mimi na wewe tunapaswa kuifanyia kazi kwa uzito katika maisha yetu sasa kama viongozi au watawala. Na hicho ndicho kitakachoangaliwa na kukumbukwa baada yetu.

Asante sana!

CEO - ujasiriamaliafya

Hakuna maoni: