Katika biashara ya aina yoyote mzalishaji hana budi afahamu mambo kadhaa ya msingi yatakayomsaidia kufanya maamuzi ya kumuwezesha kupata faida ya juu katika biashara anayoifanya:
Kwanza kabisa ajiulize kama bidhaa anayozalisha ina soko? Na kama soko lipo:
- Lipo wapi na hali ya miundombinu za kulifikia iko vipi ( ili afahamu gharama ya kufika sokoni kama utaamua kuuzia sokoni).
- Bidhaa inahitajika kwa wingi kiasi gani na wakati gani sokoni
- Soko linahitaji bidhaa yenye sifa zipi ( ubora n.k. ili uzalishe sawa na matakwa ya soko n.k)
- Kama wanunuzi watakuwa na utayari kununulia unakozalishia, je unao uwezo wa kutosheleza mahitaji yao (ili uweze kujipanga kukidhi mahitaji kwa kuongeza uzalishaji au kwa kuungana na wazalishaji wengine).
- Linganisha bei ya bidhaa sokoni na bei ya kuuzia unakozalishia (ili ujue palipo na faida zaidi kwako baada ya kuondoa gharama za kufuata soko) Ila ukiamua kuuzia sokoni hakikisha unao uwezo wa kushindana na wauzaji wengine huko sokoni.
Majibu ya maswali haya ndiyo yatakayokupa msingi wa kujipanga kiuzalishaji ili hatimaye upate faida. Hivyo hata kabla hujaanza kuzalisha fahamu haya yaliyotajwa hapa juu. Kutafuta na kutumia taarifa za masoko ya sehemu tofauti.
Kwa kadri utakavyokuwa unaendelea kuzalisha, mabadiliko mbali mbali yatatokea kuhusiana na uzalishaji wako na hata kuhusiana na soko la bidhaa unayozalisha kwa maana ya kuku.
Ili uendane na mabadiliko yanayotokea ni muhimu mzalishaji upate taarifa za hali ya soko mara kwa mara. Taarifa hizi zitakusaidia kufanya maamuzi yatakayo kuwezesha kuendelea kupata faida.
Taarifa za masoko zinaweza kupatikna kwa wazalishaji kadhaa kuungana na kuunda umoja wao. Katika umoja huo wawakilishi wachache wanakuwa na jukumu la kutafuta taarifa za masoko ya kuku sehemu mbali mbali ambako kunaweza kuwapa wazalishaji tija zaidi.
Walio katika umoja huo watatumia taarifa hizo kufanya maamuzi ya kuuza kwa faida zaidi kwa pamoja au kwa mmojammoja kutegemeana na hali halisi. Watoa taarifa pia watafanya mawasiliano ya kuwajulisha wanunuzi juu ya upatikanaji wa kuku kwenye maeneo wanakozalishiwa.
Mbinu zaidi ya kupata masoko mazuri
Umoja wa kuzalisha na kuuza
Kwa kawaida kama bidhaa ina soko, wateja hupatikana kwa urahisi pale wanapohakikishiwa upatikanaji wa bidhaa kwa wingi katika sehemu moja.
Katika hali hii, wanunuzi huwa tayari hata kununua kwa bei ya juu zaidi kwa sababu ya kupunguza muda na gharama ya kutafuta bidhaa ya kutosha kupeleka sokoni.
Kwa upande wa kuku jambo hili linawezekana kama mfugaji atafuga kuku wengi wa umri usiopishana sana kwa wakati mmoja. Watakapofikia kimo kinachofaa kuuza utawauza wengi kwa wakati mmoja na kwa faida zaidi.
Mahali ambapo mfugaji mmoja mmoja hawezi kukidhi wingi wa hitaji la wanunuzi,wafugaji kadhaa wanaweza kuunda umoja wao wa kuzalisha (kila mmoja kwake ) na kuuza kwa kipindi kimoja na kupata faida zilizotajwa hapa juu.
Faida nyingine ya kuuza katika umoja ni kuongezeka kwa uwezo wenu wa kupanga na kusimamia bei mnayotaka kuuzia. Sauti na uamuzi wenu wa pamoja utawapa nguvu ya kusimamia bei yenu mnayoipanga dhidi ya bei za chini wanazotaka wanunuzi. Uwezo wako wa kusimamia bei unyoitaka ni mdogo ukiuza peke yako.
Source: RLDC
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni