Jumatano, 14 Desemba 2016

Kuzaliana na kutotolesha Vifaranga

Uchaguzi wa Kuku bora
Ili upate kundi lenye kuku bora huna budi uchague jogoo bora na matetea bora wa kuzalisha kundi lako.

Angalia sifa zifuatazo unapochagua:
• Tetea na jogoo wawe na umbo kubwa.
• Wanaokua haraka.
• Wenye uwezo wa kustahimili magonjwa.
• Matetea wanaoweza kutaga mayai mengi.
• Matetea wanaweza kuatamia na hatimaye kutotoa vifarangakwa wingi na kuvilea.
• Jogoo unaowachagua kwa ajili ya matetea au makoo yako wasiwe na uhusiano wa
damu.

Ukiishachagua wazazi wa kundi lako changanya jogoo na matetea kwa uwiano wa jogoo mmoja kwa matetea 10 hadi 12. Ukiwa na matetea 20 utahitaji kuwa na jogoo wawili.

  • Nchini kwetu zipo aina tofauti za kuku wa asili ambao wana sifa tofauti. Wafugaji wengi hufuga kutegemeana na uwezo wa kuku kuhimili magonjwa ,kuwa na uzito mkubwa, utagaji wa mayai mengi n.k. Koo za kuku wa asili wenye sifa za namna hii ni aina ya Bukini , Kuchi, Kuchere na wa Kawaida wasio na ukoo maalum. Hawa kwa ujumla wao wakitunzwa vizuri wana uwezo wa kufanya vyema katika mazingira ya ya nchi hii kwa sababu wameishayazoea. 

Kuatamia na kuangua mayai:
Baada ya jogoo kupanda matetea au makoo, hawa watataga mayai. Mayai yanaweza kutotoleshwa kwa njia ya asili au kwa kutumia vifaa vya kutotolesha.

Kutotoa kwa njia ya asili
Hii inafanyika kwa kuku kuatamia mayai kwa hatua zifuatazo.

Kuandaa kiota:
  • Kiota kiandaliwe kabla kuku hajaanza kutaga kwa kukiwekea nyasi kavu na kuzisambaza kwa kutengeneza muundo wa kata au sahani iliyozama kidogo.
  • Kiota kinyunyiziwe dawa ya unga kuua wadudu kabla na baada ya kuweka nyasi. Iwapo kuku atajiandalia kiota chake mahali panapofaa aachwe hapo ila kiota kiwekewe dawa ya kudhibiti wadudu.

Ufugaji wa nusu huria
Maandalizi ya kuku anayetaka kuatamia
Dalili za kuku anayetaka kuatamia ni:
  • Anatoa sauti ya kuatamia.
  • Ushungi wake umesinyaa.
  • Hapendi kuondoka kwenye kiota.
  • Hupenda kujikusanyia mayai mengi


Kuku wenye dalili za kutaka kuanza kuatamia akaguliwe ili kuhakikisha kuwa hawana wadudu kama utitiri, chawa, viroboto n.k. wanaoweza kumsumbua wakati wa kuatamia. Akiwa na wadudu watamsumbua hataweza kutulia kwenye kiota na kuatamia vizuri. Matokeo yake ataangua vifaranga wachache. Hivyo walio na wadudu wanyunyizie dawa ya unga kabla hawajaanza kuatamia ili kudhibiti tatizo hili.

Kuatamia
Kuku anapotaga mayai yaondolewe na kubakiza moja kwenye kiota ili kumwita kuku kuendelea kutaga. Kuku akiwa tayari kuatamia awekewe mayai kwa kuatamia. Kwa kawaida kuku mmoja anaweza kuatamia vizuri mayai 10 hadi 13 kwa wakati mmoja.

Kipindi cha kuangua mayai ni kuanzia siku 20 baada ya kuatamia. Ukitaka kutotolesha vifaranga wengi kwa wakati mmoja, kuku akianza kutaga yakusaye mayai yake na kumbakizia yai moja ili aendelee kutaga.Mayai utakayokusanya yaweke mahali pasipo na mwanga mwingi na penye ubaridi kiasi.

Fanya hivi kwa kuku kadhaa wanaotaga ndani ya muda unaokaribiana. Kila atakayeonyesha dalili ya kuanza kuatamia muwekee mayai kati ya 10 na 12 aatamie. Kwa njia hii wataatamia na kuangua ndani ya kipindi kimoja. Na utapata vifaranga wengi wa umri mmoja hatimaye kuuza kuku wengi kwa pamoja.

Kulea vifaranga kwa kumtumia kuku
Kulea Vifaranga
Baada ya vifaranga kutotolewa waache na  mama yao                   mahali penye usalama kwa muda wa mwezi moja mbali na mwewe, vicheche, paka, kenge, n.k. Hakikisha wanapata maji na
chakula cha kutosha muda wote. Kulea vifaranga kwa kumtumia kuku
Njia nyingine ni kuwaweka vifaranga mahali pazuri na kuwafunika na tenga ili kuzuia mwewe wakati wa mchana kwa kuhakikisha
kuwa hawapigwi na jua wala kunyeshewa mvua.Wakati wa usiku warejeshe kwa mama yao ili awakinge na baridi. Fanya hivi hadi
wafi kie umri wa mwezi mmoja ndipo uwatenge na mama yao.
Pia unaweza kutumia kifaa maalum cha kulelea vifaranga (kitalu) mara baada ya kuanguliwa. Katika kitalu wanapatiwa joto wanalohitaji. Kifaa hiki kinaweza kutengenezwakwa karatasi ngumu itumikayo kutengeza dari.(angalia mchoro unaofuata).
Kulea vifaranga kwa kumtumia kitalu

Au
Katika mazingira ya kijijini unaweza
kutengeneza wigo wa mduara kwa magunia.
Upana wake uwiane na wingi wa vifaranga
ulionao na kina chake kama mita moja. Ukuta
wake uwe na tabaka mbili za magunia hayo
zilizoachana kwa nafasi ya inchi tatu au
nne. Kati kati ya nafasi hiyo jaza maranda ya
mbao au pumba za mpunga. Tayari utakuwa
umepata kitalu cha kulelea vifaranga.

Ndani ya kitalu weka taa ya chemli ya kutoa joto linalohitajika kwa vifaranga.

Fuatilia tabia ya vifaranga wanapokuwa katika kitalu.

Wakiisogelea sana taa ina maana joto halitoshi, ongezea joto kwa kupandisha utambi. Wakienda mbali sana na taa, joto limezidi punguza. Kitalu kikiwa na joto zuri vifaranga watatawanyika kote katika kitalu na kuonyesha kuchangamka.
Mama yao akitengwa na vifaranga arudishwe kwenye kundi lenye jogoo, atapandwa na kurudia kutaga mapema. Kwa njia hii kundi la kuku litakuwa kubwa kwa muda mfupi. Kwa kawaida vifaranga wengi hufa kabla ya kufikisha miezi miwili kutokana na baridi, kuliwa na wanyama wengine na magonjwa.

Ili kudhibiti magonjwa, vifaranga wapewe chanjo dhidi ya magonjwa yafuatayo:
  1. Kideri ( New castle) siku ya 3 baada ya kuanguliwa, rudia baada ya wiki tatu kisha uchanje kila baada ya miezi mitatu.
  2. Kuhara damu au rangi ya ugoro (Coccidiosis) : Wapewe kinga kwa dawa ya Amprolium kwa siku 3 mfululizo wanapofikisha umri wasiku 7 baada ya kuanguliwa.
  3. Gumboro wanashusha mbawa na kujikusanya pamoja kwa baridi, pia wanaharisha nyeupe.Hutokea kuanzia wiki ya 2 hadi ya 18.Wapewe chanjo siku ya 10 hadi ya 14 baada ya kuanguliwa na rudia baada ya siku 28 na 42. Kwa magonjwa mengine angalia maelekezo sehemu ya magonjwa ndani ya mwongozo huu sura zitakazofuata.

Vifaranga wapewe chakula kilichoelezwa katika sehemu ya hii yamuongozo huu na maji safi ya kutosha wakati wote kwa muda wa miezi miwili. Baada ya hapo wanapewa chakula cha kuku wanaokua.
Kuku wakikaribia kupevuka wakiwa na miezi mitatu hadi minne tenganisha temba na majogoo ili kudhibiti kuku wenye uhusiano wa damu wasipandane wao kwa wao. Wakipandana na mayai yao yakianguliwa hawatatoka vifaranga wenye sifa nzuri mfano: ukuaji wao utakuwa hafifu kuliko wazazi wao, uwezo mdogo kuhimili magonjwa na wengine wanaweza kuwa na ulemavu. Pia zingatia matemba hao wasipandwe na baba
yao. Vilevile majogoo hao wasimpande mama yao.


Source: RLDC

Hakuna maoni: