Jumatano, 14 Desemba 2016

Banda Bora La Kuku


Sifa za banda bora la Kuku
Ukiamua kufuga katika banda kwa njia mbili zilizoelezwa awali utatakiwa kujenga banda
lenye sifa zitakazokidhi mahitaji ya msingi ya kuku. Banda bora la kuku linatakiwa kuwa
kama ifuatavyo:

Liwe jengo imara
  •  Pasiwe na sehemu zilizo wazi kwenye msingi na kati ya ukuta na paa.
  •  Banda lijengwe na vifaa vinavyopatikana katika mazingira yako ili liwe na gharama utakayoweza kumudu.
  •  Unaweza kutumia matofali ya udongo, udongo, miti, fito,n.k. Ukitumia fito au mabanzi ondoa maganda ili kuthibiti mchwa.
  • Jengo imara litazuia maadui kama panya, vicheche, paka, nyoka na wezi kuingia ndani ya banda na kuwadhuru au kuwaiba kuku.
Liwe rahisi kusafisha
• Kuta na sakafu visiribwe zisiwe na nyufa ili kurahisisha kusafisha.
• Pia itadhibiti kusiwe na wadudu wa kujificha katika nyufa kama papasi, viroboto n.k.
• Sakafu ya banda lazima iwekewe matandazo kama pumba ya mpunga au maranda
ya mbao au mabaki ya mazao au nyasi kavu kutegemeana na kinachopatikana kwa
urahisi katika mazingira yako.
• Matandazo haya husaidia kunyonya unyevu unaotokana na kinyesi cha kuku au maji
yanayomwagika katika banda.
• Banda hubakia kavu bila kuwa na harufu mbaya na wadudu kama inzi hata vimelea
vya magonjwa hudhibitiwa.
Eneo la nje kuzunguka banda kuwe na usafi wa kudumu
Hali ya usafi nje ya banda itafanya wadudu kama siafu au mchwa na wanyama kama panya na paka mwitu wakose maficho. Nje ya banda ndani ya uzio kuwe na miti midogo na mimea mingine midogo kwa ajili ya kivuli.
Ufugaji nusu huria
Ufugaji wa nusu huria
Liwe na nafasi ya kutosha kwa kuku waliopo:      
Kwa kawaida eneo la mita mraba moja hutosha
kuku wanne wanaotaga au kuku 8 wa nyama.
Nafasi ya mita mraba 1 inatosha vifaranga 16
hadi kufikia umri wa majuma manne.

Liweze kuingiza hewa na mwanga wa
kutosha: Banda linaloweza kuingiza hewa
safi na kutoka ndani yake hubaki kavu. Harufu
mbaya hutoka na kuku huweza kupumua hewa
safi. Hii husaidia pia kudhibiti kuzaliana kwa
vimelea vinavyosababisha magonjwa,hivyo
hudhibiti magonjwa.
Lisiwe na joto sana au baridi sana: Panda miti ya kuzunguka banda lako ili eneo liwe
na kivuli cha kutosha na pia lisiwe na upepo mkali.Kama hali halisi ya eneo la kufugia ina
joto kubwa kwa vipindi virefu paa la banda wakati wa ujenzi liinuliwe juu zaidi kuruhusu
mzunguko zaidi wa hewa na joto la paa ( kama ni la bati) liwe mbali juu ya kuku.
Joto kwenye banda linaweza kusababishwa na msongamano wa kuku, hivyo mfugaji
aangalie aweke idadi ya kuku inayowiana na ukubwa wa banda lake.
Paa
Paa lifunike ukuta kwa sehemu kubwa
Liwe imara na lisilovuja. Waweza kutumia mabati,       
 nyasi, madebe, makuti n.k. kutegemeana na
upatikanaji wa vifaa vya kuezekea.Wakati wa 
kuezeka paa lisiishie karibu sana na ukuta bali
liwe na sehemu kubwa iliyozidi ukuta kuzuia 
mvua kuingia ndani kama ni ya upepo ( angalia
mchoro hapa chini).
Vifaa vinavyohitajika katika banda la kuku
Kuku wakifugwa kwa mtindo wa nusu ndani na nusu nje wanahitaji huduma mbalimbali
ndani ya banda na ndani ya wigo. Ili kutoa huduma hizi vifaa vifuatavyo ni muhimu viwe
katika banda:
Vyombo vya Maji
Kinywesheo cha kujitengenezea
Kinywesheo
Kuna njia nyingi za kutengeneza vyombo vya kuwekea maji kuku ya kunywa.
• Aina ya mojawapo unayoweza kutumia ndoo au debe la lita kumi au ishirini ya plastiki. Kata ndoo hiyo pande nne 
kutoa nafasi ya kuku ya kunywea kama kielelezo kinavyoonyesha. Tengeneza idadi ya vyombo hivi inayowiana na wingi wa kuku ulionao.
           
• Au waweza kutumia sufuria au beseni pana kiasi. Hii huwekewa tofali au jiwe safi pana baada ya kuwekewa maji ya kunywa ili kuzuia kuku wadogo wasizame na maji yasichafi liwe kirahisi.
• Vifaa maalum vya kunyweshea kuku vinapatikana katika maduka ya pembejeo zakilimo.
Vyombo vya Chakula
Vyombo hivi ni muhimu viwe vimetengenezwa vizuri ili visiwe chanzo cha upoteaji wa chakula.
Unapotengeneza kilishio cha kuku kumbuka kuwa kuku wana tabia ya kuchakura. Husambaza
au kupekua chakula kwa miguu hata kwa midomo ili kupata chakula cha chini.
Kilishio
                       
Tabia hii husababisha kumwagwa kwa chakula kingi chini na kusababisha hasara. Unaweza kudhibiti tatizo hili kwa kutengeneza vyombo visivyoruhusu kuku kuchakura kama inavyoonyeshwa kwenye kielelezo hapa chini.
Unaweza kutengeneza kilishio hiki wewe mwenyewe au fundi seremala waliopo katika eneo unaloishi. Inafaa kilishio kiwe chembamba ili kuku wasiweze kuingia. Pia kinatakiwa kiwe kirefu ili kuku waweze kula bila kusongamana.
Viota
Zipo aina tofauti za viota ambazo hutumika kwa ajili ya kutagia. Ipo aina ya ambayo ni
ya kutagia kuku mmoja mmoja. Vipimo vinavyopendekezwa kwa kila kiota ni upana wa
sentimita 30, urefu sentimita 30 na kina sentimita 35. Upande wa mbele uachwe waziila sentimita 10 za kwanza kutoka chini zizibwe na ubao ( angalia kielelezo). Weka idadi ya viota inayotosheleza
kuku ulio nao.
Muunganiko wa Viota
Pia ipo aina nyingine inayoweza kutumiwa na kuku zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja. Ni kama kiota
kimoja kilichogawanywa katika vyumba kadhaa. Ila kila chumba kina vipimo kama vya kiota kimoja(
angalia picha hapa chini).Aina hii ya kiota ina upana wa sentimita 30 na kina sentimeta 35 na urefu wake unategemea idadi ya viota.
                          
Viota vinatakiwa kuwa na giza ili kuku wasiogope kuingia kutaga ndani yake. Pia giza
husaidia kupunguza tabia ya kuku kula mayai na kudonoana. Kiota kinafaa kuwekwa
mahali ambako ni rahisi kuku kuingia na kutoka. Vile vile iwe ni sehemu itakayorahisisha
usafishaji wa kiota chenyewe.
Vichanja
Kuku wana asili ya kupenda kulala au kupumzika sehemu iliyoinuka. Hivyo ndani ya
banda weka vichanja vitakavyotosheleza idadi ya kuku waliopo.
         

Hakuna maoni: