Jumamosi, 24 Septemba 2016

SIRI MIA MBILI (200) ZA MAFANIKIO KATIKA MAISHA.



Leo ndugu msomaji na mfuatiliaji wa makala za Ujasiriamali na Afya naomba tuanze kuangalia siri mia mbili za mafanikio.
Mafanikio yoyote tunayoyaona kwa wale waliotangulia kufanikiwa yana siri au kitu ambacho mwingine si rahisi kufahamu. Ni makusudi yangu basi tushirikiane kuchambua siri mia mbili ambazo wengi waliozizingatia na kuzifanya kuwa sehemu ya maisha yao wamebadilika na kubadili kabisa historia ya maisha yao. Siri hizi nitazichambua mojamoja na ni imani yangu kuwa ukizifuatilia kwa makini wewe nawe historia ya maisha yako itabadilika kabisa. Ninalokuomba tangu sasa badili mtizamo wako na kuamini kuwa sasa unaenda kufanikiwa kimaisha na kiafya kabisa. 

  1. Dhibiti muda wako wa kulala usingizi (sleep less); Kudhibiti muda wa kulala usingizi kwa kulala kidogo ni uwekezaji mkubwa sana katika maisha ambao unamalipo makubwa sana na huongeza uzalishaji kwa kiwango cha juu sana. Watu wengi hawahitaji masaa zaidi ya sita kulala kwa lengo la kuimarisha afya zao. Jaribu kujiwekea utaratibu wa kuamka mapema kwa saa 1 kila siku kwa siku 21 kinyume na mazoea yako. Hili litakujengea tabia na kuimarisha afya yako. Usingizi unaohitajika kwa afya ni ule wa thamani na si wingi wa masaa ya kulala. Fikiria katika mwezi mzima ukawa na masaa ya ziada 30 na ukayatumia kwa mambo ya msingi au ya maendeleo.
  2. Tenga saa moja kila asubuhi kwaajili ya shughuli ya maendeleo yako binafsi; Tafakari,pata taswira ya siku unayoiendea, soma jumbe zinazokupa ari na maongozi kwa siku unayoiendea, sikiliza mikanda au video zinazokupa hamasa au soma falsafa za watu mashuhuri. Tumia muda huu kuhuisha na kujipa moyo kwa uzalishaji wa siku yako. Angalia jua linapochomoza walao mara moja kwa wiki na anza siku kwa mtizamo chanya. Kuanza siku kwa mtizamo chanya ni mbinu kubwa sana inayoweza kukufanya kufikia malengo yako na kufanya mambo yako kwa uhakika zaidi.
  3. Usiruhusu mada ambazo hazina tija kwa mafanikio yako kutawala au kuwa na nguvu zaidi ya shughuli zako ulizojipangia kuzifanya. Jiulize mwenyewe kila siku “je ninautumia muda wangu na rasilimali zangu nyingine vizuri? Matumizi mazuri ya muda ni matumizi mazuri ya maisha yako na hukuongezea umakini katika utendaji wako.
  4. Tumia kanuni ya mpira/manati yaani “rubber band” kujiongeza kimawazo kulenga kufikia malengo uliyojiwekea katika maisha yako yatokanayo na mtizamo chanya wa mafanikio. Usiruhusu kabisa akili yako kutafakari vitu ambavyo havina manufaa kwako na kwa kila unachotafakari jiulize mwisho wa kutafakari kuna mafanikio yoyote? Nguvu ya kujitambua kiakili inakusaidia pale unapopata mawazo ya kukuumiza au kukusononesha ghafla utapata ujasiri na kuruhusu akili yako kutafakari vitu vyenye manufaa. Jiulize wakati wote “Je akili yangu ipo sawa?”
  5. Ukipigiwa simu hata kwa mtu usiyemjua ipokee kwa shauku na kuonesha heshima kwa aliyekupigia. Mfano kama simu ya aliyekupigia huifahamu na ni simu yako binafsi waweza pokea kama ifuatavyo, ‘Mtega hapa; nani mwenzangu? au au kama ni ya ofisini Ofisi ya MtegaGFA hapa; nikusaidie tafadhali!’ Na unapopokea simu hakikisha umesimama au umetulia ili kuifanya sauti yako iwe ya kimamlaka au kibiashara.
  6. Kwa siku nzima tunakutana na mawazo mazuri na mabaya, na kawaida ukipata wazo zuri usipolinukuu katika “note book” yako likiingia jipya lile la mwanzo linapotea. Hivyo basi jitahidi kuandika katika “note book” au “card” ili kutunza kumbukumbu ya wazo lolote jipya la mafanikio unalokutana nalo katika shughuli zako za kila siku. Viandikio hivyo vinapatikana katika maduka ya shajala na ni bei ndogo sana. Na ukifika nyumbani kumbuka kuweka kumbukumbu vizuri za mawazo yale uliyoyapata na kuyapitia upya. Hii ni sawa na Oliver Wendell Holmes alivyosema “Man's mind, once stretched by a new idea, never regains its original dimensions”.
  7. Jiwekee utaratibu wa kila Jumapili jioni kupangilia mambo unayokusudia kufanya kwa wiki zima linalofuatia na uwe na nidhamu binafsi katika kuhakikisha yote uliyopanga kwa wiki zima unatekeleza bila kizuizi chochote. Hii itakusaidia kufahamu ni vikwazo vipi umekumbana navyo wiki iliyotangulia jinsi ya kuboresha na kufanya vizuri zaidi wiki linalofuatia. Itakutia moyo binafsi na kukufanya uione kazi yako vizuri.
  8. Wakati wote kumbuka msingi huu;- Ubora wa maisha yako ni Ubora wa mawasiliano yako. Jinsi gani unawasiliana na watu wengine, na zaidi unavyowasiliana na hisia zako binafsi. Kile akili yako inalenga kukifikia ndicho utakachofikia, ukiwa na mtizamo hasi na matokeo yatakuwa hasi bila shaka na hii ni sheria au kanuni ya asili ya binadamu yeyote.
  9. Simamia kusudi lako na si matokeo. Kwa lugha rahisi, fanya jambo lolote kwa furaha kwa kuwa umekusudia kulifanya ili likusaidie wewe au litamsaidia mwingine au kwasababu ni kitu cha thamani. Usilifanye kwa kuwekea kipaumbele FEDHA au KUHESHIMIWA, fedha na heshima vinakuja vyenyewe na hii ndivyo dunia inavyokwenda.
  10. Tafuta mazingira yatakayo kufanya ufurahi kidogo kwa siku. Mfano kwa kujiangalia tuu katika kioo chako asubuhi ucheke hata kwa dakika tano tuu. Kicheko kinazalisha kemikali ambazo ni za muhimu sana na zinazotufanya tuishi kwa furaha wakati wote. Kicheko pia kinaufanya mwili kuwa vizuri. Kicheko au furaha hutumika kama tiba kwa watu walio na udhaifu mbalimbali na hasa wa akili na simanzi. Mtoto mdogo wa wastani wa umri wa miaka 4 kwa siku anafurahi au anacheka mara 500 na wastani mtu mzima anashauriwa kucheka au kufurahi mara 15. Jenga mazingira ya kufurahi au kucheka hakika utaongeza uhai au siku zako za kuishi.
Kwa leo naishia hapa,
\\Mtega GFA
georgemtega@gmail.com au +255 625 843 804
Endelea kufuatilia mambo haya kupitia www.ujasiriamaliafya.blogspot.com

Hakuna maoni: