Alhamisi, 5 Januari 2017

IJUE NJIA YA MAFANIKIO



Heri ya Mwaka mpya ndugu yangu na msomaji wa makala zetu za “ujasiriamaliafya” kwanza napenda kutumia nafasi hii kukupongeza wewe binafsi pamoja na familia yako yote kwamba hatimaye tumepata kibali kwa yeye aliyetupa pumzi hii kuuona mwaka 2017.  Mungu akubariki sana na ninakutakia mwendo salama katika njia yako ya mafanikio katika mwaka huu wa 2017. “HAPPY NEW YEAR 2017” na “HERI YA MWAKA MPYA 2017”.
Tofauti na tulivyozoea leo katika andiko langu nitajaribu kutumia nukuu za Biblia kwani mimi kwa neema niliyopewa ni mwanafunzi wa Biblia pia. Hata hivyo kwa kuthamini imani za watu wengine wasiotumia Biblia naomba tuchukuliane hivyo kwani ni muhimu kufahamu katika uchambuzi wa mambo mbalimbali nukuu kutoka vyanzo mbalimbali pia zinahitajika sana ili kutufanya tuelewe maarifa haya kuwa si kitu kipya sana bali ni katika kukumbushana kwa nia ya kutufanya tuende vyema katika safari yetu ya mafanikio.
Mungu Muumbaji wetu sisi binadamu anahitaji kuona kila mmoja anafanikiwa na katika kukamilisha mapenzi hayo kwetu ametutengenezea njia pia kwa kila mmoja kumfanya afanikiwe.
Mungu anapenda kila mmoja aishi maisha yenye mahusiano na yeye, yaani tuishi mbali na masumbufu mbalimbali, tuwe na familia njema, tuwe na kipato kizuri, tuishi na jamii inayotuzunguka iliyofanikiwa n.k.
Sasa basi katika kukamilisha hili upo uwekezaji ambao Mungu ameufanya kwa kila mmoja wetu. Ndani yako kuna uwekezaji uliofanywa na Mungu siku ile ulipoumbwa. Hakuna mmoja wapo yeyote aliyeumbwa na Mungu akaachwa tupu. Wewe siyo MTUPU uko uwekezaji uliofanywa na Mungu ndani ya kila mmoja. Uwekezaji huo ni wa vitu sita vifuatavyo;-
  1. Maisha: Kila mmoja anazaliwa na anaishi sawa sawa. Tunazaliwa, tunakua hadi tunafikia uzee hatua hizi za maisha kila mmoja anapitia.
  2. Muda: Katika siku moja tuna masaa 24 na kila mmoja anayatumia masaa hayo hakuna mmoja anayeweza kusema amepewa masaa mengi zaidi au pungufu zaidi ya mwingine wote tuna masaa yanayolingana.
  3. Kipaji na Uwezo: Kila mmoja ana kipaji au uwezo aliowekewa ndani mwake unaomtofautisha huyu na yule.
  4. Neema ya Kumuwezesha: Kila mmoja amewekewa kitu ndani yake cha kumfanya atende au afanye jambo ambalo hatimaye atagundua si kwa uwezo wake wala nguvu zake bali upo msaada usioonekana uliomfanikisha jambo lile.
  5. Ahadi: Zipo ahadi ambazo Mungu ametoa kwa kila mmoja bila upendeleo na uwezekano wa kuzipokea ahadi hizo. Mfano ahadi za uzima, chakula, mavazi, hekima, maarifa, n.k. 3Yohana 1:2 “mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako ....”
  6. Fursa: Kila siku ni mpya ndiyo maana kuna sekunde, dakika, siku, wiki, miezi, miaka na vyote havifanani kabisa.
Sasa mgogoro upo kwenye namna kila mmoja anavyoutumia uwekezaji huo. Na matokeo ndiyo yanatupa majibu ya ni namna gani huyu au yule ametumia uwekezaji uliomo ndani mwake. Maana majibu ni dhahiri kabisa!!!
Ndugu yangu fahamu hatujaumbwa na Mungu kama roboti, kama tungeumbwa na Mungu kama roboti kila jambo lingefanywa nasi kulingana na Mungu alivyoweka programu ndani mwetu lakini tangu mwanzo anatuonesha kuwa baada ya kutuumba alitupa vitu vitatu vya kutuongoza katika njia ya mafanikio MWANZO. 2: 15-17;-
  1. Uhuru wa kuamua: Tumepewa uhuru binafsi wa kuamua ili tutofautishwe na roboti.
  2. Dhamiri ya kutuongoza: Kila mtu anaye mtu wa ndani asiyeonekana kwa macho ambaye utaisikia sauti yake akikwambia fanya hivi au vile. Hiyo ndiyo dhamiri.
  3. Uhuru wa Kuchagua: Kila mmoja ana uhuru wa kuchagua; unaweza kuchagua ulale siku nzima au usilale, umchague kiongozi yupi na yupi umuache na hapa ndipo kwenye hatari maana unaweza kumchagua fisi awe kiongozi au sokwe au usichague kabisa.
Upo jinsi ulivyo kwa kuwa umechagua uwe jinsi ulivyo na nikuhakikikishie hakuna unayepaswa kumlaumu, kwamba nipo jinsi nilivyo kwasababu ya serikali, au kwasababu ya wazazi wangu, au kwasababu ya mume wangu, au mke wangu, au watoto wangu , au walimu wangu, au mchungaji wangu, au shule yangu, au chochote, n.k. HAPANA umechagua mwenyewe uwe jinsi ulivyo.
Kila mmoja ana wajibu binafsi wa namna anataka maisha yake yaende. Kumlaumu yeyote ni kukwepa wajibu wako binafsi. Wewe binafsi unawajibika kwa hayo usiyoyataka.
Mwingine utasikia anasema Nchi yetu ni masikini, au wilaya yangu ni masikini, au familia yetu ni masikini; NIKUULIZE SWALI; Je kuna nchi inayozalisha umasikini? Au kuna wilaya, au familia inayozalisha umasikini? Hii ni kukwepa kuwajibika kwa kila mmoja binafsi.
Unao uhuru wa kuchagua umasikini au kuchagua utajiri. Na matokeo ya kuchagua ulichochagua ndiyo yamekuweka uwe ulivyo.
Mafanikio hayaji kwa kusoma na kuchagua misingi miwili au mitatu ili kufanya mageuzi ya maisha yako na nikuhakikishie kwamba kama maisha uliyonayo unayachukia amua kugeuka kabisa na ubadili uelekeo kama kufanya “engine overhaul” unapangua vyote usivyovitaka na kuweka unavyovitaka na kuanza safari ya mafanikio sasa.!!!! Hapa si Mungu wa kukugeuza ni wewe kuamua kufanya “engine overhaul” ya safari yako ya mafanikio maana hayo ni matokeo ya uhuru wako binafsi. Ukisema tangu sasa inawezekana mimi kuwa tajiri maana yake umasikini umeshindwa. Maana upo huru kuwa tajiri au kuwa masikini.
Mafanikio siyo sehemu Fulani, mafanikio ni safari ndefu tena isiyo na mwisho; huwezi kufika mahali alafu ukasema sasa nimefanikiwa. Ni safari unayoenda hatua kwa hatua na ni ndefu sana, haina mwisho.
Katika safari hii ya mafanikio vipo vitu unavyopaswa kusafiri navyo ili kuifanikisha safari ya mafanikio;-
Ni lazima utembee na utayari: katika 1Samweli 16:7 katika mistari hii Mungu inatwambia Mungu haangalii sura ya nje, anaangalia utayari wako ndani katika kukufanikisha kwenye safari yako. Sura ya nje inadanganya sana ndugu yangu Mungu anataka;-
  • Moyo wa unyenyekevu kwenye safari hiyo.
  • Utayari wa kukubali makosa yako.
  • Utayari wa kujifunza.
  • Ni lazima utembee na lengo mahususi: Hatupo hapa kwa bahati mbaya, tupo hapa kwa mpango maalum wa Mungu.
  • Uushikilie vizuri muda wako uliombele.
  • Tengeneza taswira ya maisha yako, unataka maisha ya namna gani?
  • Amua unataka ukumbukwe kwa lipi baada ya maisha haya?
Itaendelea kipindi kijacho.........

Hakuna maoni: