Jumatatu, 19 Desemba 2016

Mbinu bora za uzalishaji wa mbegu za mahindi

Mbinu bora za uzalishaji wambegu za mahindi
 
Ili kupata mbegu bora na safi yenye vinasaba vyake halisi na isiyokuwa na uchafu wo-wote wa nje ni muhimu wakulima wafahamu na kufuata utaratibu wa ki - agronomia (kanuni za kilimo bora) katika uzalishaji wa mbegu. Zifuatazo ni kanuni na mbinu bora, za uzalishaji wa mbegu bora za mahindi.

Hatua ya 1: Kuandaa shamba 
  • Eneo la kupanda mbegu za mahindi lazima litengwe umbali wa mita 200 kutoka shamba lingine litakalopandwa mahindi na mkulima mwenyewe au wenzake kijijini. Hatua hii hulenga kuzuia uchafu wa kijenetiki kutokana na mwingiliano wa mbegu kwa njia ya uchavushaji wa asili ambao hutokea bila kuhusisha binadamu moja kwa moja. Angalizo: Mzalishaji wa mbegu asipotenga shamba la mbegu kwa umbali huu itapelekea mbegu zake kupoteza uasili na ubora kwani zitakuwa na baadhi ya sifa za mahindi yaliyopandwa jirani na shamba hilo la mbegu.
Hatua ya 2: Kulima
  • Shamba lifyekwe (liandaliwe) mapema kabla ya msimu wa mvua,
  • Lilimwe vizuri kwa kutumia nyenzo zilizo ndani ya uwezo wa mkulima.
  • Magugu yote yaondolewe,
  • Lisiwe na mabonge makubwa ya udongo, na ni vizuri sana lisiwe na visiki
  • Lisiwe limepandwa mahindi msimu uliopita ili kuondoa tatizo la maotea, magonjwa na wadudu waharibifu kwenye shamba la mbegu.

Hatua ya 3: Kuandaa pembejeo
Maandalizi ya pembejeo na vifaa vingine yafanyike mapema. Pembejeo na vifaa hivyo ni pamoja na:
  • Mbegu mama: Mbegu mama ni ile ambayo mkulima anataka aizalishe kitaalamu ili aje kuitumia kama mbegu. Sharti mbegu hii iwe imehakikiwa ubora wake na imekubalika na jamii.
  • Mbolea: Andaa mbolea sahihi kwa ajili ya kupandia na kukuzia mbegu.
  • Andaa vifaa vya kupandia kama vile kamba ya kunyooshea mistari na vijiti vya kupimia nafasi kati ya mstari hadi mstari na mmea hadi mmea.

Hatua ya 4: Kupanda
Mara mvua za kutosha na za uhakika zikinyesha, panda. Vipimo vya kupandia ni kama ifuatavyo:
  • Mstari hadi mstari: sentimeta 75 (futi 2 na nusu)
  • Mmea hadi mmea: sentimeta 30
  • Punje moja kila shimo.

Maelekezo muhimu
  • Tumia kamba ili kuhakikisha unapanda kwa vipimo sahihi. Ekari moja ya mahindi iliyopandwa kwa vipimo sahihi itakuwa na mimea 18,000.
  • Shimo liwe na kina cha sentimeta 10 hadi 12, mbolea iwekwe kwanza, halafu ifukiwe kidogo kwa udongo, kisha ifuatie mbegu halafu udongo kidogo wa kufunika mbegu.

Hatua ya 5: Weka Mbolea
Mahindi ya mbegu lazima yatunzwe vizuri na yapewe lishe ya kutosha, ili mimea ikue vizuri na masuke yawe makubwa na yaliyojaa.

Maelekezo muhimu kuhusu mbolea:
Tumia mbolea ya samadi au mboji iliyoozeshwa na kuhifadhiwa vizuri. Ili kuongeza ufanisi mbolea iwekewe kwenye mistari au mashimo ya kupandia mbegu. Inakadiriwa kuwa kiasi cha mbolea kinachohitajika ni tani 8 kwa ekari moja.

Mbolea za asili hasa samadi iliyoozeshwa vizuri inafaa sana kwa kupandia na kukuzia mbegu. Makadirio ya mbolea ni kiasi cha viganja viwili kwa shimo.

Pale itakapolazimu, mkulima anaweza kuchanganya mbolea za asili na mbolea sahihi za viwandani kupandia na kukuzia mbegu.

Hatua ya 6: Usafi wa shamba
Shamba la mbegu halitakiwi kuwa na magugu hata kidogo kwa wakati wote. Hivyo ni vyema lipaliliwe mara 3 au 4 kulingana na mahitaji. Swala la msingi ni: shamba lisiwe na magugu hadi kuvuna.

Hatua ya 7: Kuondoa mimea isiyofaa
Kagua shamba kila wakati na:
  • Ondoa mimea yote isiyofanana na mbegu husika kwa kuikata na kuiondoa shambani kabla ya kutoa mbelewele.
  • Ondoa mimea yote yenye dalili za magonjwa ya mashina, mizizi, na majani na ichome ili kuuwa wadudu waharibifu na kudhibiti magonjwa.
  • Dhibiti wadudu, magonjwa na wanyama waharibifu kwa kutumia mbinu na madawa ya asili. Ikilazimu tumia dawa sahihi za viwandani. Kwa kawaida, dawa inawekwa kabla mahindi hayajafunga.

Hatua ya 8: Kuchagua mbegu
Mbegu zinachaguliwa mimea ikiwa shambani na baada ya kuvunwa.

Uchaguzi wa mbegu shambani:
Uchaguzi wa mbegu huanzia shambani hata kabla ya kuvuna. Kazi hii hufanyika mahindi yakiwa yameshabeba, masuke yanaonekana lakini majani hayajakauka. Katika hatua hii mkulima anatakiwa achague mimea yenye sifa zifuatazo:
  • Haina magonjwa
  • Ina mahindi makubwa yaliyojifunga hadi mwisho
  • Ina urefu wa wastani (kwepa mifupi sana au mirefu sana)
  • Ina mabua manene
  • Bua halijaanguka au kuvunjika
  • Inafanana na wenzake wengi
  • Haiko pembeni ya shamba
Mimea itakayochaguliwa ni ile iliyo ndani ya shamba na kuacha mimea yote ya pembeni ya shamba. Ili kutambua mimea uliyoichagua kama mbegu, weka alama kwa kutumia vitambaa au vipande vya kamba ya rangi, funga kwa kukaza kwenye mimea husika karibu na mhindi ili visidondoke kwa upepo. Hii inamaanisha kuwa sio mimea yote shambani ina sifa ya kuwa mbegu.

Uchaguzi wa mbegu baada ya kuvuna
Mahindi yanapokauka vizuri:
Hatua ya 1: Vuna mahindi yale ya pembeni mwa shamba na yale yote ambayo hayakuchaguliwa katika ile hatua ya uchaguzi wa mbegu shambani. Mahindi haya yatengwe sehemu ya pekee ili yasije yakachanganyikana na mbegu.
Hatua ya 2: Vuna mahindi yale yaliyochaguliwa kama mbegu. Mahindi haya yatengwe mbali na mahindi mengine. Mahindi haya yasambazwe ili yakauke vizuri kwa mwanga wa jua. Baada ya mahindi hayo kukauka vizuri:

Chagua mahindi yenye sifa zifuatazo:
  • Makubwa, yenye mistari mingi
  • Yasiyo na mapengo ya kutojaza
  • Yasiyo na dalili zozote za punje zilizooza
  • Yaliyojaza hadi mwisho wa gunzi

Baada ya uchaguzi:
• Pukuchua mahindi yaliyochaguliwa
• Weka dawa (za asili au viwandani) kuzuia wadudu waharibifu
• Hifadhi kwenye mifuko au magunia yanayopitisha hewa vizuri

Tahadhari!!
  • Mifuko yenye mbegu isiwekwe sakafuni kwani kwa kufanya hivyo, mbegu zitaharibika kwa kunyonya unyevu. Unaweza kuandaa fremu ya mbao au mabanzi au miti ili mifuko iwe angalau futi moja kutoka kwenye sakafu. Mbegu pia zinaweza kuhifadhiwa katika benki za mbegu za wakulima ama benki mazao.
  • Zuia mbegu isinyeshewe mvua
  • Zuia panya kwa kutumia mitego au paka
  • Pale ambapo dawa ya viwandani itatumika, ikishawekwa kwenye mbegu zisitumike tena kama chakula kwa sababu ni sumu kali sana.
HONGERA!!! BAADA YA KUPITIA HATUA ZOTE SASA UNA MBEGU
BORA TAYARI KWA KUPANDA MSIMU UNAOFUATA AU KUUZA
KAMA UMESAJILIWA
Source: PELUM - TZ

Hakuna maoni: