Alhamisi, 8 Desemba 2016

Maadui wawili wakubwa!

Leo nataka tujadili maadui wakubwa wawili wa furaha na jinsi tunavyoweza kuepuka maadui hawa ili tuweze kuwa na maisha ya furaha. Kikubwa utakachoona hapa leo ni kwamba maadui hawa wa furaha wanaanza na sisi wenyewe, kama ambavyo furaha inaanza na sisi wenyewe.

Adui wa kwanza ni ubinafsi.

Huwezi kuwa na furaha kama unakuwa mbinafsi. Ubinafsi ni pale ambapo unajiangalia wewe pekee na kutojali kuhusu wengine. Unatumia muda mwingi kufikiria mambo yako na kuona namna gani utawazidi wengine. Ubinafsi unatufanya tuwe na ulimwengu wetu wenyewe.

Ubinafsi unaua kabisa furaha kwa sababu mara nyingi hutujengea hali ya kushindana na wengine. Unapokua mbinafsi, unaangalia ni nini wewe unacho na wengine wana nini. Kama wengine wana zaidi ya ulichonacho wewe utajiona hufai na huwezi kama wengine. Hali hii itakuzuia wewe kuwa na furaha.

Unapokuwa mbinafsi, ukikutana na changamoto unaona maisha yako ndiyo hayafai, utaona kila mtu ana maisha mazuri kasoro wewe pekee, na hapo ndipo utajikuta ukiona maisha hayana maana kwako.

Ufanye nini?

Acha kuwa mbinafsi, acha kujifikiria wewe mwenyewe na acha kuona kama wewe pekee ndiye uliyepo hapa duniani. Chochote unachofanya, jali wengine pia. Usifanye kitu kwa sababu tu wewe unapata unachotaka, bali fanya ukijua kuna mchango mkubwa unatoa kwa wengine. Fanya ukijua kuna maana unatoa kwa wengine, na hili litakufanya uone maisha yako yana maana na kuwa na furaha.

Unapoacha ubinafsi na kushirikiana na wengine, utaona namna kila mtu anavyopitia changamoto kwenye maisha yake, hata pale utakapopitia changamoto, hutakata tamaa kwa sababu unajua kila mtu anapitia changamoto za namba hiyo. Utajua kila mtu anapigana vita yake na siyo wewe mwenyewe. Hii inakupa nguvu ya kuendelea na mapambano.

Unapoacha ubinafsi watu watapenda kushirikiana na wewe na kwa pamoja mtaweza kufanya makubwa.

Adui wa pili ni tamaa.

Tamaa ni adui mkubwa sana wa furaha, kwa sababu tamaa haina mwisho. Hata ufanye nini, kama una tamaa, hutaweza kuitimiza tamaa yako.

Unapokuwa na tamaa, chochote unachopata, unaona bado hakitoshi. Ni sawa na unapokuwa na tamaa ya fedha, unaweza kusema nikipata milioni kumi basi maisha yangu yatakuwa safi, unazipata milioni kumi, unagundua bado hazikutoshi, unafikiria milioni 100 ukizipata bado hazikutoshi, unafikiria bilioni. Tuelewane hapa, kuwa na malengo ya kifedha yanayokua siyo vibaya, vibaya ni pale unapoendeshwa na tamaa katika kupata fedha hizo, unashindwa kuishi maisha yako mengine kwa sababu unaendeshwa na tamaa hii ya kupata kiasi hicho cha fedha. Na kwa sababu tamaa ina nguvu, utajikuta unatumia njia ambazo siyo sahihi kupata kile unachotaka.

Tamaa inakuzuia kufurahia na kushukuru kwa kile ulichopata, kwa sababu bado kuna vingi zaidi ambavyo bado hujapata. Hakuna kiwango chochote cha kitu kinaweza kutosheleza tamaa.

Ufanye nini?

Ondokana na tamaa, badili sababu yako ya kutaka kupata kile unachotaka. Kama ni fedha, angalia sababu hasa inayokusukuma kupata fedha, isiwe tamaa zako binafsi, badala yake iwe mchango unaotoa kwa wengine mfano bidhaa au huduma bora, au pia nafasi za kazi kama umeajiri.

Ridhika na shukuru kwa kila unachopata, hata kama ni kidogo kiasi gani, jua siyo wote wanaoweza kupata, hivyo ni muhimu kwako kushukuru. Thamini kila unachopata kwenye maisha yako, usichukulie vitu kwa mazoea, na wala usijaribu kushindana na wengine kwa namna yoyote ile. Kuwa na ndoto zako, kuwa na malengo yako na yafanyie kazi. Furahia kila hatua unayopiga na songa mbele zaidi.

Hao ndiyo maadui wakubwa wawili wa kuepuka katika maisha yetu kama tunataka kuwa na furaha ya kudumu kwenye maisha. Kama ambavyo tumeona, kila kitu kinaanzia ndani yetu, furaha na hata maadui wa furaha. Hivyo tuna nafasi kubwa ya kujenga maisha ya furaha kwetu sisi wenyewe. Fanyia kazi haya unayojifunza kwenye FALSAFA MPYA YA MAISHA na utakuwa na maisha bora kila siku.

Salatiel Chaula

Hakuna maoni: